10 Mei 2025 - 22:08
Source: Parstoday
Mfumo wa THAAD wa Marekani ulioko Israel wafeli kuzuia makombora ya Yemen

Kombora lililovurumishwa kutoka Yemen limefika katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel huku mfumo wa ulinzi wa anga wa THAAD wa Marekani ukishindwa tena, na kulazimisha mamilioni ya Wazayuni kukimbilia katika mahandaki wakiwa na hofu na wahka.

Kombora hilo lililovurumishwa Ijumaa, limesababisha ving'ora vya tahadhari kusikika katika jiji la Tel Aviv na “maeneo mengine zaidi ya 200."

Operesheni hiyo ililazimisha utawala huo kuamuru kuwashwa kwa mifumo yake ya makombora ya ulinzi, ikiwemo mfumo wa ulinzi wa anga wa THAAD unaotengenezwa Marekani, kituo cha habari cha utawala huo Channel 14 kiliripoti.

Kwa mujibu wa kituo hicho, mfumo huo wa makombora, hata hivyo, ulishindwa kuzuia kombora hilo, na kufanya kuwa “mara ya pili” kwa kifaa hicho cha gharama kubwa kushindwa kukabiliana na makombora ya Yemen.

Vyombo mbalimbali vya habari vya Israel, kwa upande mwingine, viliripoti milipuko mashariki mwa Tel Aviv na katika mji mtakatifu unaokaliwa kwa mabavu wa al-Quds, ambako mfumo wa THAAD ulijaribu kuzuia kombora hilo bila mafanikio.

Gazeti la Israeli la Yedioth Ahronoth liliripoti kuwa safari za ndege katika uwanja muhimu wa Ben Gurion zilisimamishwa.

Jeshi la Yemen limekuwa likitekeleza operesheni za kulipiza kisasi kwa niaba ya Wapalestina Gaza na kuweka mzingiro wa baharini dhidi ya meli na vyombo vya majini vya Israel vinavyoelekea katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu tangu Oktoba 2023.

Wakati huo huo, Sayyid Abdul-Malik Badr al-Din al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameeleza kuwa, jamii za Kiarabu na Umma wa Kiislamu zinabeba jukumu la msingi la mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza akisisitiza matokeo mabaya ya kutochukua kwao hatua.

Aidha amelaani mauaji ya kimbari yanayoendelea kutekelezwa na utawala katili wa Israel huko Gaza, na kuyataja kuwa "uhalifu wa karne." Kiongozi huyo wa Ansarullah ya Yemen ameonyesha masikitiko makubwa kutokana na mwitikio hasi wa mamilioni ya Waislamu kwa ukatili wa kila siku unaowakabili watu wa Palestina. Matamshi ya Al-Houthi ni kilio cha hadharnia kwa Ummah wa Kiislamu kuamka katika majukumu yao na kuchukua msimamo dhidi ya dhulma.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha